Sunday, July 2, 2017

KILIMO BORA CHA MAHINDI.



KILIMO BORA CHA MAHINDI


KUANDAA SHAMBA, KUPANDA NA KUPALILIA

Kuandaa Shamba, Kusafisha, Kulima/Kutifua

Ni vyema mashamba yaandaliwe mapema kabla ya msimu wa kupanda haujaanza ili kumpa mkulima fursa ya kupanda kwa wakati unaotakiwa. Kuna njia mbalimbali zinazotumika kuandaa mashamba. Kati ya njia hizi ni pamoja na kufyeka, kung’oa visiki na kulima. Shamba linaweza kulimwa kwa kutumia:

Jembe la mkono - wengi wanatumiaJembe la kukokotwa na wanyama kama ng’ombePower tillersMatrekta


Matumizi ya trekta, power tillers na jembe la kukokotwa na wanyama yanapunguza nguvu kazi kwani vinachimbua udongo na kuufanya kuwa tifutifu (kufanya isiwe na mabonge makubwa, wala isiwe vumbi vumbi). Hii husaidia:

Mizizi ya mimea kupenyeza ardhini kirahisiUdongo kuweza kuhifadhi majiUdongo kuwa na hewa inayohitajika na mimeaUkuaji mzuri wa mimea hivyo kuongeza mavuno


Mbegu Bora za mahindi

Matumizi ya mbegu bora ni muhimu katika upatikanaji wa mavuno mengi na bora. Kuna makundi mawili makuu ya mbegu ambayo ni:

Mbegu za asili: Ni zile ambazo zimetumika miaka mingi katika historia ya kilimoMbegu zilizoboreshwa: Hizi ni zile zilizoboreshwa kutoka mbegu za asili. Kundi hili linagawanywa kwenye makundi mawili - composite varieties na mbegu chotara (Hybrids).


Ushauri wa matumizi ya mbegu zilizoboreshwa unatofautiana kutoka eneo moja na lingine kwa sababu ya:

Mwinuko kutoka usawa wa bahariKiasi cha mvua katika eneo husikaMuda unaotumia mbegu hadi kukomaa


Mbegu za mahindi zilizoboreshwa ni kama TMV1, TAN 250, TAN 254, Staha, Situka na zingine zote zinazoanza na herufi “H” kama vile H 250, H 251 na H 615. Pia mbegu mpya zilizotangawa na Kamati ya Taifa ya Mbegu mwaka huu ni WE4102, WE4106, WE4110, WE4114, WE4115 kutoka ARI ILONGA.


Jinsi Ya Kuweka Mbolea Za Kupandia

Mbolea hizi zinawekwa shambani kabla ya kupanda/kusia mbegu. Zinawekwa kwa njia mbalimbali kama vile kusambaza kwenye eneo husika na kuchanganya na udongo, au kuweka kwenye mistari au mashimo ya kupandia. Ni bora zaidi kuchanganya mbolea za Minjigu Phosphate au Minjingu Mazao na udongo kuliko kutia kwenye shimo la kupandia. Pia kuchanganya mbolea na udongo huondoa athari za mbolea kwenye uotaji wa mbegu, hasa kama kuna uhaba wa unyevunyevu.


Viwango Vya Mbolea Za Kupandia mahindi

Kiwango cha mbolea za kupandia kilichopendekezwa ni kilo 20 fosfati (P) kwa hektari ambayo ni sawasawa na kiasi cha mifuko 2 ya DAP (= mfuko mmoja kwa ekari). Ikiwa mbolea ya minjingu phosphate itatumika basi mifuko mitatu itatosa kwa hekta (= mfuko mmoja na nusu kwa ekari). Na endapo utaamua kuitumia mbolea ya minjingu mazao basi tumia mifuko minne na nusu kwenye hekta moja au mifuko miwili kwa ekari moja.


Upandaji wa mahindi

Muda wa kupanda: Kulingana na msimu mahindi hupandwa mwanzonimwa mwezi wa 11 baada ya mvua za kwanza kunyesha (specifically from 1st to 15th day of November) ambayo huvunwa mwezi Machi mwishoni au aprili mwanzoni. Pia mahindi hupandwa mwanzoni mwa mvua za masika yaani mwezi wa pili mwishoni na mwezi wa tatu mwanzoni ambayo huvunwa mwezi Julai katikati na Agosti mwanzoni. Katika msimu huu utayarishaji wa shamba hufanyika mwezi wa pili mwanzoni.
Muda wa kupanda unatofautiana kutoka eneo moja kwenda jingine kulingana na majira ya mvua. Kwa mfano katika wilaya ya Morogoro tarehe za kupanda ni kuanzia februari 15 hadi Machi 15. Mkulima anashauriwa afuate kalenda ya muda wa kupanda kama anavyoshauriwa na bwana shamba wake.


Nafasi ya kupandia mahindi

Kupanda kwa nafasi ni kati ya njia bora za kilimo inayomwezesha mkulima kupata mazao bora. Hivyo ni muhimu sana kuzingatia kupanda kwa mistari na kufuata nafasi zinazoshauriwa na wataalamu wa kilimo. Zifuatazo ni nafasi za kupanda mahindi na idadi ya mbegu kwa kila shimo na kiasi cha mbolea (kwa vizibo vya soda) inayotakiwa kuwekwa kwa shimo:

Kwa nafasi ya 90 sm X 30 sm, panda mbegu moja na uweke kizibo kimoja cha mboleaKwa nafasi ya 90 sm X 25 sm, panda mbegu moja na uweke kizibo kimoja cha mboleaKwa nafasi ya 90 sm X 50 sm, panda mbegu mbili na uweke vizibo viwili vya mbolea


Kupalilia

Ni muhimu shamba lipaliliwe baada ya mimea kuota ili kuondoa magugu. Magugu ni mimea hivyo hushindana na mimea iliyopandwa na mkulima kwa kunyonya virutubisho ardhini. Magugu yanaweza pia kuhifadhi wadudu na magonjwa yanayoweza kushambulia mimea iliyopandwa na hivyo kupunguza mavuno. Magugu yaweza kuondolewa wa palizi ya mkono (yaani) kung’olea (ikiwa magugu yapo mbali mbali sana) au kulima kwa jembe la mkono au kwa kutumia dawa/viuagugu (HERBCIDES) hasa 2-4D.


Mbolea za kukuzia mahindi

Ni mbolea zinazotumika baada ya mimea kuota kwa lengo la kuikuza mimea ili itoe mavuno bora. Mara nyingi mbolea hizi zinatoa kirutubisho cha naitrojeni. zifuatazo ni mbolea za kukuzia na kiwango chake cha naitrojeni:

UREA: 46% NCalcium Ammonium Nitrate, CAN: 23% NSulphate of Ammonia, SA: 21%


Urea inakirutubisho cha naitrojeni (N) kwa kiwango kikubwa na watu wengi wanauzoefu nayo. Vilevile bei yake ni nafuu ikilinganishwa na mbolea zingine za kukuzia. Mbolea hii iko katika hali ya chengachenga za mviringo (granules) za rangi nyeupe. Kiwango cha urea ni nusu kizibo cha soda kwa kila shina. Mbolea hizi hazidumu kwenye udongo kwa muda mrefu kwa hiyo huwekwa shambani wakati mimea inapokuwa na mahitaji makubwa ya kirutubisho cha naitrojeni na wakati udongo una unyevunyevu na shamba halina magugu.


Pia wakulima hutumia mbolea za kukuzia zinazopatikana kwa bei nafuu kama vile BOOSTER (foliage nitrogeneous fertilizers) ambayo hupigwa kwa kunyunyizia katika majani ya mmea kila baada ya wiki 3, kwa mara 2-3 mpaka mahindi kuvunwa. Kiwango cha kupiga ni mchanganyo wa mls 50-80 ktk lita 15 za maji. Mbolea za kukuzia huwekwa kuzunguka kila shina la mimea au pande mbili au tatu au nne za kila shina. Cha muhimu ni kwamba mbolea isirundikwe sehemu mmoja. Minjingu Mazao (kg 50/ekari = gramu 10kwa shimo) pia yaweza tumika kwa kukuzia, hivyo mkulima yko huru kuchagua kulingana na uwezo na upatikanaji wake.

Viwango Vya Mbolea Za Kukuzia Vinavyoshauriwa

Kiwango kinachopendekezwa ni kilo 60 naitrogeni kwa hektari, ambacho ni sawasawa na kiasi cha mifuko miwili ikiwa utatumia UREA. Hata hivyo mbolea zingine kama SA inaweza kutumika kama kuna mahitaji ya salfa. Hivyo basi utumie mifuko mitatu kwa hekta ambayo ni sawa na mfuko mmoja kwa ekari. CAN inaweza kutumika kama kuna mahitaji maalum ya nitrate na ammonium na endapo utaitumia basi mifuko minne na nusu itatosha kwa hekta, ambapo kwa ekari moja utatumia mifuko miwili tu.


Kwenye mahindi mbolea ya kukuzia inawekwa baada ya palizi ya kwanza ambayo ni kama wiki tatu mpaka wiki nne baada ya kupanda. Kwa kila mmea mmoja weka kiasi hiki cha mbolea:

UREA: kizibo kimoja cha sodaCAN: vizibo viwili vya soda, na SA: kizibo kimoja cha soda


Mambo Muhimu Ya Kuzingatia

Kuweka mbolea: Sehemu za nchi ambazo muda wa kukua mahindi ni mrefu (zaidi ya miezi mitatu), ni vyema kuweka mbolea za kukuzia mara mbili, yaani nusu ya kiwango kinachopendekezwa baada ya mwezi mmoja, na kurudia tena (kutumia nusu iliyosalia) baada ya wiki tatu.


Kupalilia: Katika kilimo cha mahindi, ni muhimu shamba lipaliliwe siku 14 hadi 21 baada ya mimea kuota kufuatana na hali ya shamba wakati wa kupanda. Wataalamu wanashauri kwamba katika kilimo cha mahindi, shamba lipaliliwe mara 2-3, kufuatana na hali ya magugu katika shamba.


Shamba la mahindi ambalo halijapaliliwa linaweza kupunguza mavuno kwa asilimia 60 hadi 100 ya mavuno yanayotarajiwa. Hata kama mkulima atatumia mbegu bora, aina na kiasi cha mbolea zinazoshauriwa, kupanda kwa mstari pamoja na mbinu nyingine bora zinazoshauriwa, bila kupalilia hali hii itaathiri mavuno yake.

Kudhibiti magonjwa na wadudu.

Magonjwa Yanayoshambulia Mahindi

i) Maize streak virus

Dawa/Kudhibiti: Mbegu bora inayostahimili ugonjwa, kupanda mapema, kung’oa mimea iliyoathirika ama kunyunyiza dawa za kuua ‘vectors’ kama vile inzi weupe (white flies).


Maize streak virus


ii) Smut (Fugwe)

Dawa/Kudhibiti: Tumia Helerat ukifuata maagizo kamili.


iii) Cob rot (kuoza kwa mhindi)

Dawa/Kudhibiti: Tumia mbegu zinazostahimili kuoza.


Muhindi uliooza

Yafahamu magonjwa sumbufu ya vitunguu maji

Wadudu Na Wanyama Wanaoshambulia Mahindi

a) Viwavi Jeshi

Ni wadudu aina ya funza ambao hutokana na Nondo.Hushambulia mahindi kwa kula majaniyake pamoja na shina. Wadudu hawa huangamizwa/kudhibitiwa kwa njia zifuatazo;-

Kuondoa vichaka karibu na shambaKunyunyizia sumu za asili kama vile Mwarobaini majuma mawili ya mwanzo.Kunyunyizia sumu za viwandani endapo wadudu wameanza kuonekana kama vile Karate 1ml/1L


Viwavi jeshi


b) Funza wa Mabua (Maize Stalk Borer)

Funza wa mabua hutoboa shina la mahindi na kusababisha kudumaa kwa mahindi.

Matundu, ungaunga kama wa msumeno huonekana kwenye majani yaliyoathiriwa.Mashambulizi huanza juma la pili hadi la tatu baada ya mahindi kuota.Njia za kudhibiti zinazotumikaKuchanganya mahindi na mazao jamii ya mikunde km vile maharagweKung’oa mahindi yaliyoshambuliwaSumu za asili mwarobainiSumu za viwandani km vile Karate. pia waweza tumia Malathion, sumithion, vumbi ya cymbush au Sevin 5G na ufuate maagizo kamili.


c) Cutworms (Vikata Shina)

Dawa/Kudhibiti: Tumia Dragnet FT na ufuate maagizo kamili.


d) Wanyama waharibifu

Kudhibiti: Kuwatishia na kuwafukuza wanyama, kama vile Nyani, Tumbili, Ngedere.

Ili mkulima aweze kupata mazao mengi na bora inashauriwa kutumia dawa za kuzuia magonjwa na wadudu washambuliao mimea na njia zinginezo.

KUVUNA, KUKAUSHA, KUSAFISHA NA KUHIFADIHI

Kuvuna

Mahindi yako tayari kuvuna wakati kikonyo kimekuwa dhaifu na mahindi yanaangalia chini. Mahindi yakishakauka vizuri yanatenganishwa na bua halafu majani ya mhindi kutolewa.


Kukausha

Kama mahindi hayajakauka vizuri hukaushwa zaidi katika juani siku 3-4 ili kupunguza unyevunyevu kufikia kiwango kinachofaa kwa kuhifadhi (14%). Ni muhimu mahindi yakauke vizuri ili yasioze yakiwekwa ghalani. Ili kujua kama mahindi yamekauka vizuri, tia mahindi kadhaa kwenye chupa ya soda iliyokauka na uongeze kiganja kimoja cha chumvi. Tingisha chupa halafu uwache itulie kwa dakika tatu. Chumvi ikikwama kando ya chupa, basi mahindi hayajakauka vizuri.



Kusafisha

Mahindi yaliyokauka vizuri hupepetwa na vilevile mahindi mabovu huondolewa.


Kuhifadhi

Mahindi huhifadhiwa ghalani baada ya kuwekwa viatilifu vya kuzuia bungua wa mahindi Njia za kisasa za uhifadhi hutumiwa kama vile matumiz ya ACTELLIC SUPER DUST katika uwiano wa 1kg kwa gunia 5-10 za ujazo wa 100kg. Kiatilifu kingine ni actellic solution katika rate ya 5mls katika gunia moja la kg 100. Njia nyingine ya kienyeji katika kuhifadhi mahindi ni kuweka juu ya ghala ambalo chini yake kuna jiko la kupikia ambalo hutoa moshi unaotumika kufukuza na kuua wadudu.

No comments:

Post a Comment

HABARI NJEMA KWA WAKULIMA, NAFAKA BADO YASHIKILIA PALE PALE.

Hali ya soko masokoni katika masoko makuu ya mikoani hapa nchi bado iko vizuri, ambapo mazao hayajapanda wala kushuka kulinganisha na wiki i...