Wednesday, July 12, 2017

KILIMO CHA MIGOMBA (NDIZI)

KILIMO CHA MIGOMBA (NDIZI)

Utangulizi
Niukweli usiopingika kuwa kilimo cha migomba(ndizi) hapa Tanzania kimekuwepo kwa miaka mingi sana iliyopita.Kilimo hichi kimejizolea umaarufu sana sababu zao la ndizi linalopatikana kwenye migomba limekuwa likitumiwa na jamii na sehemu kubwa ya inchi yetu kwa chakula.Baadhi ya mikoa inayolima
zao hili ni:

Kilimanjaro,
Kagera,
Mbeya,
Arusha,
Manyara,
Mara,
Tanga,
Morogoro n.k

Zao la ndizi pamoja kuwa ni zao la kibiashara kwa soko la ndani bado njia bora zikitumika katika kuzalisha migomba inayotoa ndizi zinazokidhi vigezo vya uhitaji wa soko la nje itasaidia zaidi kukuza vipato vya wafanyabiashara husika na kunufaisha taifa pia si kwa biashara ya ndizi kwa hapa inchini bali na nje ya mipaka ya inchi yetu.

Matumizi
Kilimo cha migomba(ndizi) kina faida nyingi,baadhi ya faida za migomba katika zao la ndizi ni:
Zao la chakula,
Zao la biashara,
Kutengeneza pombe,
Kulisha mifugo,
Kutengeneza mbolea(mboji),
Matandazwa shambani,
Kutoa kivuli,
Malighafi ya kutengenezea vyakula na vinywaji mbalimbali.

Uzalishaji
Zao la ndizi likizalishwa kwa utaalamu unaokubalika huweza kutoa mazao yenye ubora wa hali ya juu na kuongeza uzalishaji wa kukidhi haja ya soko.Katika uzalishaji wa zao hili ni vyema kuzingatia mambo yafuatayo:

1. Hali ya hewa
Kiasi cha chini cha mvua kifaacho ni 100mm kwa mwezi au 1200mm kwa mwaka.Mwinuko kutoka usawa wa bahari ni mpaka mita 1800,zaidi ya mita hizo migomba haikui vizuri.Kiasi cha joto kinachofaa ni nyuzi joto za sentigredi 25 hadi 30 chini ya nyuzi joto 16 migomba haikui vizuri.
Mgomba hustawi zaidi kwenye:
Udongo wenye rutuba ya kutosha,
Usiotuamisha maji na usio na chumvi,
Chachu ya udongo inafaa iwe kati ya pH 5 mpaka pH 8.

1. Aina za ndizi
Ni vyema kufahamu kuwa kwa inchini Tanzania kuna aina nyingi za ndizi.Ndizi hizi zinaweza kugawanywa katika makundi yafuatayo :

Aina ambazo huliwa kwa kuchomwa,kukaangwa na kupikwa.
Aina ambazo huliwa baada ya kuvundikwa(huliwa kama matunda).
Kwa ujumla katika kufahamu aina za majina ya ndizi ambazo zinapatikana inchini mwetu, ni kama ifuatavyo:
Mzuzu,
Mshale,
Matoke,
Bokoboko,
Mkono wa Tembo,
Bukoba,
Kisukari,
Kimalindi,
Mtwike n.k

Kuna aina nyingine za ndizi ambazo kwa sasa huzalishwa hapa nchini ambazo zina fahamika kwa ubora wake katika masoko ya ndizi ya kimataifa. Aina hizi ni pamoja na:
Williams,
Grand Naine,
Pazz,
Jamaica,
Gold Finger,
Uganda green,
Embwailuma Giant,
Chinese Cavendish.

1. Utayarishaji wa shamba
Hakikisha unasafisha eneo husika kwa kutumia zana zinazotakiwa.Hakikisha unangoa visiki na mizizi yote .Lima sehemu hiyo kwa kutumia jembe la mkono, rato, au trekta ili kuwezesha mizizi laini ya migomba kupenya ardhini kwa urahisi. Baada ya visiki na magugu yote kuondolewa na hivyo ardhi kuwa wazi, uchimbaji wa mashimo ya kupandikiza machipukizi au miche ya migomba unaweza kufanyika.

1. Nafasi ya kuchimba mashimo
Kawaida migomba inaweza kupandwa kwa utaratibu ufuatao:
kwa nafasi ya umbali wa mita 2.75 kwa 2.75, kigezo hiki mara nyingi kinakuwa kwa migomba mifupi.
umbali wa mita 3 kwa 3, kwa migomba ya urefu wa kati.
umbali wa mita 3.6 kwa 3.6, kwa migomba mirefu zaidi

1. Uchimbaji wa mashimo
Uchimbaji mashimo inafaa ufanywe mapema kabla ya muda wa kupanda. Shimo lichimbwe kwa kutenganisha udongo wa juu na wa chini. Vipimo vya shimo ni vyema vikazingatiwa.
Iwapo utachimba shimo la mviringo litafaa liwe na kipenyo cha sentimeta 60 hadi 90 na kina cha sentimeta 60 hadi 90. Iwapo utachimba shimo la mstatili au mraba litakuwa na urefu, upana na kina cha sentimeta 60 hadi 90, kutegemea kiasi cha mbolea kilichopo na kiasi cha kvua kinachonyesha sehemu hiyo.
Uwekaji wa mbolea hufuata mara baada ya mashimo kuwa tayari.Mbolea ya samadi iliyooza vizuri au mboji iwekwe kwenye lundo la udongo wa juu kando ya kila shimo na tayari kusubiri kuja kurudishiwa kwenyeshimo baada ya mche/machipukizi kuwekwa kwenye shimo.

1. Kuchagua machipukizi bora
Katika upandaji wa mche au chipukizi ni vyema kuzingatia vigezo vifuatavyo:
Liwe chipukizi sime ,yaani liwe na majani membamba,
Litoke kwenye migomba yenye sifa ya kuzaa mikungu mikubwa,
Liwe na afya nzuri na lisiwe na dalili ya ugonjwa,
Urefu uwe kati ya mita 1 na mita 2,
Kipenyo cha sehemu ya chini ya shina la chipukizi kiwe ni kati ya sentimita 15 mpaka 25.

1. Upandaji wa machipukizi
Wakati mzuri wakupanda machipukizi ni mwanzoni wa mwa msimu wa mvua kama kilimo chako si cha umwagiliaji.Baada ya kusimamisha mche/chipukizi hakikisha limefunikwa vizuri na udongo uliochanganywa na mbolea na hakikisha unashindilia vizuri ili mche uweze simama wima imara.
Machipukizi yanayo tarajiwa kupandwa yanatakiwa kuondolewa mizizi yote ili kudhibiti minyoofundo na fukuzi wa migomba. Pia maji ya moto au dawa kama vile furadani inaweza kutumika kuulia wadudu kwenye mizizi ya migomba.

Utunzaji wa shamba la ndizi:
(a) Uwekaji wa matandazwa (mulching)
Kazi hii ni vyema ikafanywa mara baada ya kupanda kama inawezekana. Matandazo yawe ni makavu na unene wa sentimeta 15 ili kuhifadhi unyevu, kuzuia magugu na yakioza yataongeza mbolea.

(b) Uongezaji wa mbolea
Baada kupanda ni vyema kuongeza mbolea kuzunguuka shina la migomba kila baada ya miaka miwili au mitatu. Mbolea hii inatakiwa kuchanganywa na udongo na kufunikwa kwa matandazwa.

(c) Umwagiliaji maji shambani
Migomba huhitaji maji mengi. Wakati wa kiangazi inafaa kumwagilia ili kuto kupunguza sana ukubwa na wingi wa ndizi zinazotarajiwa kuvunwa kwa mwaka.

(d) Kupunguzia machipukizi
Inashauriwa kupunguza migomba kwa kila shina na kubaki mimea mitatu tu, yaani Mgomba wenye ndizi (Mama), Mgomba mkubwa ambao bado haujazaa lakini unakaribia kuchanua (Mtoto), Mgomba mchanga uliochipua hivi karibuni ( Mjukuu)

(e) Uondoaji wa Majani Makavu
Migomba inafaa iondolewe majani yote makavu ili kuondoa uwezekano wa kuwepo mazalia ya wadudu na magonjwa, kuruhusu mionzi ya jua na kufanya urahisi wa kuhudumia shamba .Pia hufanya shamba kuonekana safi.

(f) Uondoaji wa ncha mwishoni mwa matunda
Baada ya mkungu kutoa ndizi, ua hunyauka na kubakiza ncha mwishoni mwa matunda. Ncha hizo hupaswa kuondolewa .Huduma hii husaidia kupunguza uwezekano wa kujeruhi matunda wakati wa kusafirisha jambo ambalo kupunguza ubora wa tunda.

(g) Kuweka Miega
Miega ni nguzo au kamba ambazo hutumika kuzuia migomba iliyobeba mikungu mikubwa isianguke kutokana na uzito mkubwa. Miega ni ya lazima katika sehemu zenye upepo mkali. Kazi hii inatakiwa kufanywa kwa uangalifu ili isijeruhi ndizi na mgomba wenyewe.

(h) Uondoaji wa kichombezo cha ua la kiume (Shumba)
Uondoaji wa shumba huwezesha matunda kukua vizuri, kuongezeka uzito wa mkungu pia huzuia magonjwa kama vile ugonjwa wa mnyauko wa migomba (Banana Baterial Wilt), ugonjwa wa majivu nchani mwa matunda (Cigar end rot). Ukataji hufanyika juu ya kovu la pili baada ya kichana cha mwisho, kwa kutumia kisu kikali.

Uvunaji
Zao la ndizi huweza kuanza kuvunwa katika kipindi cha miezi 9 hadi miezi 15 tangu kupandwa kwa chipukizi. Muda wa kuvunwa hutegemea hali ya hewa. Katika sehemu za joto ndizi huvunwa mapema zaidi kuliko sehemu za baridi. Pia migomba iliyopandwa kwa kutumia machipukizi huzaa mapema kuliko iliyopandwa miche iliyozalishwa kwa chupa (tissue culture)

Mtumizi ya Riboni
Riboni za rangi moja (au alama ya kamba) hufungwa kwenye migomba ya umri mmoja mara tu inapoanza kuchanua, na riboni ya rangi nyingine hufungwa kwenye migomba itakayoanza kuchanua wiki mbili hivi zinazofuata na kuendelea hivyo ili kurahisisha kuitambulisha mikungu ambayo itavunwa kwa wakati mmoja. Pia matumizi ya riboni hurahisisha utunzaji wa kumbukumbu ili kujua ni lini na ni mikungu mingapi itavunwa.

Wakati unaofaa kuvunwa
Mkungu wa ndizi huweza kuvunwa katika hatua tofauti kulingana na matumizi, aina na mahitaji ya soko. Mkungu huachwa kwenye mgomba mpaka vidole (matunda ) vimejaa.

Uzito wa mkungu hongezeka haraka katika wiki mbili za mwisho, ambapo migongo ya ndizi hutoweka.
Ndizi zinaweza kuvunwa zikiwa zimekomaa na zimeiva kwa kiasi cha asilimia 75 kwa ajili ya kusafirishwa mbali, pia zinaweza kuvunwa zikiwa kukomaa na zimeanza kuiva kwa ajili ya soko la karibu, au zikiwa zimekomaa na kuiva kabisa kwa ajili ya soko na matumizi ya nyumbani.

Njia bora ya kukata mkungu, ni ile inayohakikisha kuwa mkungu wa ndizi hauanguki chini na kuvunja, kuchubua au kuharibu ndizi, jambo ambalo litapunguza ubora wa ndizi. Ukichelewa kuvuna ndizi zinaweza kuharibiwa na ndege, wanyama, wadudu au kuibiwa.

Ubora wa ndizi
Ndizi zenye sifa nzuri sokoni ni zile ambazo zimekomaa kwa kiasi kinachotakiwa na zenye vidole vyenye urefu mzuri na visivyo na michubuko. Pia ziwe hazijashambuliwa na magonjwa wala wadudu waharibifu.

Kiasi cha mavuno
Mavuno ya ndizi hutegemea zaidi:
aina ya migomba,
hali ya hewa,
utunzaji wa mimea shambani.
Magonjwa
Ugonjwa wa hatari sana ni wa mnyauko wa migomba unaosababishwa na bakteria (Banana Bacterial Wilt). Magonjwa mengine yanayosumbua zao hili ni kuoza tunguu, ugonjwa wa panama, ugonjwa wa majivu nchani mwa tunda, Sigatoka, na Moko.

Wadudu waharibifu
Wadudu wanaosumbua zaidi hili ni Minyoo fundo (Banana nematodes), na Vifukuzi (Banana weevils).
Udhibiti wa magonjwa na wadudu waharibifu
Magonjwa na wadudu hawa huweza kuepukwa kwa kufuata kanuni bora za uzalishaji wa zao hili. kama usafi wa shamba na kuchagua chipukizi bora.Mbolea inayofaa wakati wa upandaji ni samadi kama vile kinyesi cha ng’ombe.

Maeneo ya fursa hii
Fursa hii ya biashara ya ndizi hapa inchini kwetu inaweza sambazwa sehemu nyingi kutokana na uhalisia kwamba matumizi ya ndizi kama chakula inachukua sehemu kubwa kwa baadhi ya jamii yetu ya Tanzania.Mlimaji ni vyema akamshirikisha mtaalamu wa kilimo kwaajili ya kupata mazao bora na vilevile ni vyema mkulima kufahamu soko lake.Biashara hii inaweza fanywa kwenye:

masoko mbalimbali makubwa au madogo,
supermarket na minimarkets zikiwa zimehifadhiwa vizuri,
mahoteli mbalimbali,
migahawa mikubwa na midogo,
mashule ya bweni kwaajili ya vyakula vya wanafunzi mbalimbali,
navile vile masoko ya nje.
Kusindika

No comments:

Post a Comment

HABARI NJEMA KWA WAKULIMA, NAFAKA BADO YASHIKILIA PALE PALE.

Hali ya soko masokoni katika masoko makuu ya mikoani hapa nchi bado iko vizuri, ambapo mazao hayajapanda wala kushuka kulinganisha na wiki i...