Wednesday, July 12, 2017

KUSINDIKA PILIPILI

USINDIKAJI WA PILIPILI KALI

Aina nyingi za pilipili kali (Chillies) hulimwa katika maeneo madogo katika sehemu nyingi nchini Tanzania na zao hili hulimwa kama zao la chakula na kibiashara.
Mavuno mengi ya zao la pilipili kali hupatikana kwa kuzingatia kanuni kama ifuatavyo;

Kuchagua aina ya mbegu
•  Chagua aina ya mbegu bora kulingana na mahitaji ya soko.
•  Chagua aina inayovumilia magonjwa, wadudu waharibifu na inayokomaa mapema.

Kuweka mbolea

Hakikisha udongo una rutuba ya
kutosha kwa kuweka mbolea za asili kama vile samadi na mboji iliyoiva vizuri, ambayo husaidia kuongeza rutuba ya udongo na kudhibiti wadudu waharibifu walioko ardhini
(Grubs).

  Inashauriwa kuweka kiasi cha tani nne au tano kwa hekta moja kila msimu. Pia kilimo cha mzunguko wa mazao huepusha magonjwa ya pilipili na hudumisha rutuba.

  Inashauriwa kubadilisha mazao katika eneo lililopandwa pilipili muda mrefu kwa kupanda jamii tofauti ya zao hilo kila baada ya miaka mitatu.

Kupalilia

Kupalilia mimea ya pilipili huwezesha
mimea hiyo kuweza kutumia virutubi-
shi pamoja na unyevu uliopo ardhini
kikamilifu. Palizi pia husaidia kuondoa
maficho ya wadudu waharibifu.
Kumwagilia maji

Kagua shamba mara kwa mara kuona
kama udongo una unyevu wa kutosha.
Pilipili changa huhitaji maji ya mara kwa
mara kuliko mimea ambayo imeanza
kutoa matunda.

Epuka kutumia maji
mengi kupita kiasi ambayo yatatuama
na kusababisha udongo kutopitisha
hewa ya kutosha kwa ajili ya ukuaji wa
mimea ya pilipili.

Kudhibiti magonjwa na wadudu
Pilipili hushambuliwa na magonjwa
hasa ya mnyauko unaosababishwa
na bakteria na ukungu.

 Ni muhimu
kukagua mashamba mara kwa mara
ili kubaini dalili za magonjwa na
mashambulizi ya wadudu waharibifu.
Endapo kuna dalili fanya uchunguzi wa
kina na dhibiti vyanzo vya magonjwa
kabla havijaleta madhara makubwa.
Kama kuna dalili za wadudu chun-
guza kasi ya mashambulizi na dhibiti
kwa kutumia madawa ya asili.

Maandalizi kabla ya kuvuna
pilipili
Kukagua shamba
Kagua shamba ili kuhakikisha kama
mazao yamekomaa. Pilipili kali
hukomaa katika kipindi cha miezi
mitatu tangu kupandikiza miche.

Dalili za pilipili kali zilizokomaa
Matunda ya pilipili hubadilika rangi
kutoka kijani na kuwa ya manjano
au nyekundu. Hata hivyo rangi ya
matunda yaliyoiva hutegemea aina ya
pilipili kali.

Bonyeza hapa ujue jinsi ya kusindika soya
https://kilimofaida24.blogspot.com/2017/07/jinsi-ya-kusindika-soya.html?m=1

Kuandaa vifaa vya kuvuna,
kubebea na kusafirisha pilipili
Vifaa vya kuvunia ni pamoja na vikapu
na mifuko, huku vya kusafirishia
vikiwa ni baiskeli na matoroli

Kuvuna
Uvunaji wa pilipili kali hufanyika kwa
kutumia mikono na huvunwa kwa
awamu ya siku mbili au tatu kulingana
na kasi ya ukomaaji au kuiva kwa
matunda.

Mambo ya kuzingatia wakati wa
kuvuna pilipili
Vuna pilipili zilizokomaa tu na kuacha
zile changa ziendelee kukomaa. Pili-
pili za kusindikwa zivunwe zikiwa
zimeiva.

Pili, chuma matunda ya pilipili
bila kikonyo kwa kutumia mkono.
Ni muhimu kuvuna mapema kabla
pilipili hazijakauka, kwani zikikauka
ni vigumu kutenganisha matunda na
vikonyo.

Tatu, rundika pilipili zilizovunwa
kwa ajili ya kusindika kwa muda wa
siku moja ili ziive vizuri na kupata
rangi ya aina moja (Curing).

Kusafirisha
  Baada ya kuvuna pilipili hupele-
kwa kwenye sehemu ya kusafishia,
kuchambua, kukausha na kufungasha.

Kusafisha
Pilipili zilizovunwa husafishwa kwa
kutumia maji safi ili kuondoa vumbi
na uchafu mwingine kisha huanikwa
kwenye makaushio bora yasiyoruhusu
uchafu kuingia.
Kukausha na kuchambua pilipili
kali
•  Tandaza pilipili safi kwenye sakafu
safi zenye vizuizi vya vumbi na
uchafu ili kuzuia vumbi na uchafu
kuingia kwenye pilipili safi
•  Chambua pilipili kuondoa pili-
pili zilizooza, zenye wadudu au
takataka nyingine na vikonyo
•  Geuza pilipili mara kwa mara ili
tabaka za chini ziweze kukauka
•  Pilipili zianikwe katika maeneo yali-
yotenganishwa kufuata awamu za
uvunaji. Kuchanganya pilipili ziliz-
ovunwa kwanza na zilizovunwa
kwa mara ya pili hushusha ubora
wa zao

•  Pilipili ikaushwe hadi kufikia
unyevu unaokubalika kwa hifadhi
salama ambao ni asilimia 10.
Kufungasha
Pilipili kali kavu zifungashwe kwenye
magunia safi ya juti au mifuko ya
nailoni ngumu. Vifungashio visiwe na
ukungu, wadudu na harufu mbaya
kwani vyote hivi hushusha ubora wa
zao la pilipili.

Kupanga madaraja
Madaraja ya pilipili kali hupangwa
kulingana na aina, ukubwa na rangi.
Pilipili zenye rangi moja zinang’aa,
zisizokuwa na ukungu na zilizokauka
vizuri hupewa daraja la juu na bei yake
huwa ni ya juu.

Kuhifadhi
Hifadhi pilipili iliyokaushwa sehemu
kavu na baridi. Magunia au mifuko ya
nailoni ngumu yapangwe juu ya chaga
kwa kupishanisha ili kuruhusu mzun-
guko wa hewa.

Kusindika pilipili kali
Pilipili husindikwa kupata unga wa
pilipili, sosi na lahamu.
a) Kusindika pilipili kavu kupata
unga: Pilipili kali huumiza macho na
pia harufu ikivutwa huleta mkereketo
ndani ya pua na kifua wakati wa
kusaga ili kupata unga. Inashauriwa
kuchukua tahadhari zifuatazo;
Vumbi la pilipili kali huumiza macho
hivyo inashauriwa kuvaa miwani ya
kukinga macho na vumbi hilo wakati
wa kusaga au kufungasha.

Aidha, mtu anayejishughulisha na
kazi ya kuchambua, kusaga na kufun-
gasha, anashauriwa kuvaa kinga ya
pua kuzuia hewa kali kuingia ndani ya
pua na kifuani. Vitu vingine vinavyo-
shauriwa ni pamoja na uvaaji wa glavu
za mikononi, na usafi wa vyombo na
mazingira kwa ujumla.

Vifaa
Mashine ya kusaga pilipili, mifuko, na
chekeche,
Malighafi
Pilipili kali kavu

Jinsi ya kusindika
•  Chukua pilipili kavu zilizo safi kisha
weka kwenye mashine ya kusaga na
saga kupata unga
•  Chekecha kwa kutumia chekeche
yenye matundu madogo (0.5mm)
kisha fungasha kwenye mifuko safi
ya nailoni na kisha weka kwenye
mifuko ya makaratasi
•  Unga wa pilipili pia unaweza
kufungashwa kwenye chupa za
kioo zenye mifuniko iliyo na lakiri
au karatasi za aluminium au plastiki
zinazoshauriwa kuhifadhia chakula
•  Vifungashio kwa ajili ya bidhaa za
kuuza viwe na uzito wa gramu 100,
250 na 1000 kulingana na mahitaji
ya soko
•  Vifungashio vidogo vidogo vya pili-
pili viwekwe ndani ya makasha ya
mbao au makaratasi magumu
•  Pilipili kavu iliyosagwa inaweza
kudumu kwa muda wa mwaka
mmoja bila kuharibika ama kupo-
teza ubora
Weka lebo itakayo onesha yafuatayo;
•  Jina la biashara na jina la bidhaa
•  Jina, anuani ya mtengenezaji pamoja
na uzito
•  Tarehe ya kusindika na mwisho wa
kutumika kwa bidhaa
•  Hifadhi mahali safi pakavu na
pasipo na mwanga mkali.
Matumizi
Pilipili ya unga iliyosagwa hutumika
kama kiungo kwa kuongeza ladha na
hamu ya chakula.

b) Kusindika pilipili mbichi
kupata sosi (Green Chili Sauce)
Vifaa
•  Mashine ya kusagia rojo na mabe-
seni ya kuoshea malighafi
•  Bakuli kubwa zitakazotumika kwa
ajili ya kuchanganyia rojo
•  Kijiko kikubwa cha chuma cha pua
(stainless steel) na mizani
•  Chupa za sosi za plastiki kwa ajili ya
kufungashia pamoja na kisu kikali
kisichoshika kutu.

Malighafi
•  Pilipili ndefu za kijani kilogramu
moja
•  Viazi mviringo gramu 100
•  Chumvi gramu 50
•  Siki miligramu 100
•  Maji safi na salama miligramu 100
•  Tindikali ya sitriki gramu 15
•  Chumvi maalumu aina ya sodium
benzoate gramu 72

Jinsi ya kutengeneza
•  Chagua pilipili ndefu zilizokomaa
vizuri na ambazo hazikusumbuliwa
na wadudu au magonjwa.
•  Chambua kuondoa takataka kama
majani au matawi na vilevile toa
vikonyo kwa mkono na osha
kwenye maji safi.
•  Chagua viazi mviringo vilivyo-
komaa vizuri na menya kuondoa
maganda, osha na chemsha hadi
viive.
•  Saga pilipili kwa kutumia blenda
kisha saga viazi kwa kutumia
blenda pia au ponda kwa mwiko
hadi viwe laini kabisa.
•  Mimina rojo la pilipili kwenye
bakuli kubwa kisha mimina rojo la
viazi vilivyopondwa kwenye bakuli
hilohilo lenye rojo la pilipili.
•  Changanya vizuri hadi upate
uwiano ulio mzuri kisha ongeza
gramu 15 za tindikali ya sitriki,
gramu 50 za chumvi na gramu 100
za siki
•  Changanya kwenye sosi na koroga
vizuri hadi mchanganyiko uwiane.
•  Jaza sosi kwenye chupa za plastiki,
funga na mifuniko imara
•  Weka lebo na lakiri kisha hifadhi
sehemu safi na yenye mwanga
hafifu
.
Muhimu
Zingatia usafi wakati wote wa usindi-
kaji ili kupata bidhaa bora na itakay-
oweza kuhifadhika kwa muda mrefu.
Sosi iliyosindikwa kwa njia hiyo hapo
juu huweza kuhifadhika kwa muda wa
miezi sita bila kuharibika.

c) Sosi ya pilipili zilizoiva
yenye mchanganyiko wa nyanya
(Tomato chili sauce)

Vifaa
Jiko, mizani, mashine ya kusaga rojo,
chujio, kibao cha kukatia, lebo, kisu
kikali kisichoshika kutu, mwiko,
sufuria, mabeseni ya kuoshea, kit-
ambaa safi cheupe, refraktomita na
kikombe cha kupimia uzito
Malighafi
Nyanya mbivu, sukari, chumvi, siki,
wanga wa mahindi, viungo, sodium
benzoate, maji safi na salama na unga
wa pilipili nyekundu gramu 20 kwa
kilo moja ya rojo.

Jinsi ya kutengeneza
•  Chagua nyanya bora zinazotoa rojo
nzito kama vile aina za Tanya, Roma
au Tengeru 97
•  Osha kwa maji safi na salama kisha
ondoa vikonyo na kata vipande
vipande
•  Chemsha kwa dakika tatu ili kura-
hisisha uondoaji wa maganda na
mbegu. Ipua na pooza
•  Saga kwa kutumia blenda na chuja
kuondoa mbegu na maganda
•  Pima uzito wa rojo kisha ongeza
gramu 75 za sukari kwa kilo moja ya
rojo

•  Tengeneza mchanganyiko wa
viungo ufuatao kwa kila kilo moja
ya rojo; pilipili manga gramu 3,
mdalasini gramu 3, iliki iliyosagwa
gramu 3, karafuu nzima gramu 3,
vitunguu maji gramu 50 na pilipili
nyekundu ya unga gramu 20

•  Funga viungo vyote kwenye kit-
ambaa safi cheupe na tumbukiza
kwenye rojo kisha chemsha ukiwa
unakoroga mpaka sosi ifikie nusu ya
ujazo wa awali au imekuwa nzito.
•  Ondoa kitambaa chenye viungo
kwenye sosi

•  Weka siki gramu 50 kwa kila kilo
moja ya rojo ya nyanya kisha ongeza
chumvi

•  Changanya wanga wa mahindi
gramu 10 kwenye maji kidogo
kisha ongeza ndani ya sosi huku
ukikoroga •  Chemsha kwa dakika tano kisha
ipua na weka kwenye chupa za sosi
ikiwa na joto lisilopungua nyuzi 70
za sentigredi. Funga kwenye mifuko
imara
•  Weka lebo na lakiri kisha hifadhi
sehemu yenye ubaridi na mwanga
hafifu.
Matumizi ya sosi ya nyanya na pilipili
Sosi hii ya pili na nyanya huliwa pamoja
na vyakula mbalimbali ili kuongeza
hamua ya chakula hicho.

1 comment:

  1. What are the different types of bets on the Super 6
    How to pick the bet type? What is the meaning of the odds on each NFL team to win the Super 토토사이트 6?

    ReplyDelete

HABARI NJEMA KWA WAKULIMA, NAFAKA BADO YASHIKILIA PALE PALE.

Hali ya soko masokoni katika masoko makuu ya mikoani hapa nchi bado iko vizuri, ambapo mazao hayajapanda wala kushuka kulinganisha na wiki i...